"Hivi tuinaelekea wapi?"
*WANAWAKE WAFURIKA KUPATA HUDUMA
BIASHARA huria imezua mengi. Hali kadhalika Sayansi na Tekenolojia nayo, imeleta mengi. Katika kuwaondolea kero wanawake wenye matiti yaliyosinyaa hapa nchini, wataalamu kutoka China wameanza kutoa huduma ya kunyanyua matiti hayo kwa kutumia mashine maalumu.
Wachina wamejipatia umaarufu katika kuleta bidhaa mbalimbali hapa nchini, zikiwamo za kuongeza nguvu za kiume, kupunguza uzito, kuotesha nywele, kujichubua (kumfanya mtu mweusi awe mweupe), kuongeza makalio nk.
Huduma hiyo ya kusimamisha matiti yaliyolala, imeanza kutolewa katika Saluni ya Blue Palace, iliyopo nyuma ya Shule ya Mapambano, Sinza jijini Dar es Salaam.
Haikuwa rahisi kuweza kuamini kuwa vitu kama hivi vinaweza kupatikana Tanzania. Mwananchi Jumapili lilifunga safari mpaka kwenye saluni hiyo inayomilikiwa na Sarafina Mtweve, kujionea jinsi teknolojia hiyo inavyofanya kazi.
Mbali na meneja wa saluni hiyo, Trust Mwembe, pia alikuwepo mtaalamu kutoka China aitwaye, Ciisy Pang, ni binti wa miaka 23 tu, lakini anasema kwa miaka minne amefanya kazi hiyo na kuwasaidia wanawake mbalimbali waliokuwa wakikerwa na matiti yaliyolegea au kuanguka.
Pang na kundi lake wanatoa huduma hii kwa gharama ya Sh150,000 kwa kuanzia, ingawa wanahisi gharama hizo zitapanda katika siku chache zijazo.
Jinsi matiti yanavyosimamishwa
Mashine hiyo inayoitwa ‘Beauty Machine’ ina uwezo wa kusimamisha matiti ya kila saizi kwa kuwa huambatanishwa na vibakuli (cups) kama unavyoona pichani.
Kazi kubwa ya mashine hiyo ni kuamsha misuli ambayo hushikilia nyama za matiti.
Pang anasema, zoezi la kusimamisha matiti huchukua wiki tatu mpaka sita, inategemea aina ya mteja na wakati mwingine juhudi zake.
Mtaalamu huyo ambaye anazungumza Kichina na kutafsiriwa na meneja wa saluni hiyo, anaelezea namna anavyofanya kazi ya kuyarudisha matiti kwa muda huo.
“Kwanza unapaswa ujue kuwa hatutumii dawa yoyote katika zoezi hili, mteja wetu akifika hapa, kinachotumika ni mashine tu ambayo hutumia umeme kama zilivyo dryer za nywele,
“Baada ya kumlaza katika kitanda kile, tunachukua kitu mfano wa bakuli (cups) mbili kulingana na ukubwa wa matiti yake, tunayatumbukiza humo, kisha tunawasha mashine,” anasema Pang.
Mtaalamu huyo anasema mashine hiyo ikiwashwa inavuta kama ‘vacuum’, na inaweza kuongezwa kasi au kupunguzwa kama inavyofanyika kwenye mashine za kufanyia mazoezi.
“Tunaiwasha mashine kwa muda wa dakika 45, mteja atachagua siku mbili katika wiki za kufanya zoezi hili mpaka litakapokamilika,”anasema Pang.
Tangu mashine hiyo iwasili nchini, takribani mwezi mmoja uliopita, Pang anasema ana wateja wanane anaowahudumia kwa nyakati tofauti ambao wamekiri kuwa maendeleo yanatia moyo.
Ni kweli mashine hii inasaidia?
Akizungumza kwa njia ya simu, mmoja wa wateja anayepata huduma hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina moja tu Irene anasema, ni wiki ya tatu sasa tangu aanze kupata huduma hiyo, anakiri kuwa matiti yake sasa yameanza kuwa magumu tofauti na mwanzo.
“Kusema kweli nilikuwa na matiti yaliyosinyaa wala si kulala tu kama ulivyouliza, ila naona sasa yameanza kuwa magumu na kurudi juu kidogo,” anasema Irene.
Akizungumzia ugumu anaoupata katika zoezi hilo, anasema safari za kila wiki saluni na zile dakika 45 za kukaa kwenye mashine zinamchosha, lakini kwa kuwa amedhamiria, amejitoa mpaka zoezi hilo litakapokamilika.
Matiti yanaweza kulegea tena?
Pang anasema kama matiti yanalegea kwa sababu fulani mfano uzazi wa watoto wengi, basi yanaweza kulegea tena kama mtu atajifungua na kunyonyesha kwa muda huo.Aidha anasema wanawake wenye matiti makubwa, ni rahisi kuanguka kama hawatayavalisha sidiria kwa muda mrefu.
“Wanawake wenye matiti makubwa huwa nawashauri kuvaa sidiria hasa wakati wa mchana na usiku wanaweza kuacha kuzivaa, hii inasaidia kuimarisha misuli inayoyabeba matiti,” anasema Pang.
Jamii inazungumziaje jambo hili
Baada ya kusikia kuwepo kwa mashine hii nchini, wanawake mbalimbali wamesema wanatamani kupata huduma hiyo lakini wengine, walionyesha woga juu ya matokeo yake.
“Ni kweli baada ya kunyonyesha watoto wawili sasa matiti yamelegea kabisa, natamani yarudi kama wakati ule wa usichana wangu, lakini nahofia huenda mbele ya safari nikapata madhara,” anasema Linda Masatu.
Linda anaongeza kusema kuwa ni vizuri mwanamke akawa na matiti yaliyojaa vizuri, lakini anahofia njia zinaweza kuwa na madhara, huku akisema kama ingetokea njia nyingine ya asili asingesita kuifuata.
Naye Batuli Famau, anasema mwanamke anapokuwa na matiti yaliyosinyaa mvuto wake hupungua, hata anapovaa sidiria anakuwa amebadili mwonekano wa nje tu, lakini ndani bado anakuwa vilevile.
“Mwanamke mrembo ni yule mwenye matiti mazuri, sasa inapobidi kutumia njia fulani ili yarudi kama tulipokuwa vigoli, tutafanya tu ili mradi kama njia hizo hazitatuangamiza,” anasema
Wanaume nao wameonekana kuunga mkono zoezi la kusimamisha matiti ingawa wengine hawaungi mkono utumiaji wa mashine hii.
Augustino Magara anasema: “Ni kweli mwanamke mwenye matiti magumu anavutia kuliko yaliolegea na kulala, lakini sasa tuwe makini kabla wake zetu hawajaumia katika mashine, hizi”
“Wote tunajua sababu zilizosababisha matiti ya wake zetu yalegee, sioni sababu ya kusema tunataka yaliyomagumu, tuwapende wake zetu hivi hivi na tuwape moyo,” anasema Nganara.
Dk Innocent Mosha wa Kitengo cha Patholojia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anasema ni vigumu kwa wataalamu wa afya kugundua madhara ya mashine hizo kwa haraka hadi pale uchunguzi utakapofanyika.
“Ingelikuwa mazoezi hayo yanachukua muda mfupi, kweli tungepata wasiwasi kwa kuwa, unapoisimamisha misuli kwa haraka ni lazima madhara yatokee, lakini hili la mazoezi, bado sifahamu,” anasema Dk Mosha.
Na Julieth Kulangwa, Gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment