DAVID ROBERT: Mkali wa Injili
anayetesa Channel O na MTV base
|
KATIKA miaka ya nyuma muziki wa
Injili ulidharaulika sana na mtu alipoonekana akiimba muziki huo alionekana
kama kituko kwa sababu hakuna aliyekuwa anaguswa na nyimbo hizo.
Si kwamba kipindi hicho hapakuwa
na waimbaji wazuri wa muziki huo, la hasha walikuwepo tena waliokuwa
wanafanya vizuri pengine kuliko waimbaji wa leo wanaoimba nyimbo za Injili.
Katika miaka hiyo kulikuwa na
waimbaji kama Ephraim Mwansasu, Faustine Munishi, Mungu Four, Ency Mwalukasa,
Jeniffer Mgendi na baadaye akajitokeza mwimbaji kama Cosmas Chidumule
aliyekuwa anapiga muziki wa dunia kabla hajageuzia kibao kwenye nyimbo za
injili.
Miaka hiyo ilikuwa ni mara moja
sana kusikia muziki wa injili ukipigwa katika kumbi za starehe kama baa,
kwenye harusi na mahali pengine kwenye starehe.
Lakini leo hii upepo umebadilika
ndivyo alivyoanza kusema mwanamuziki mahiri wa muziki wa injili nchini, David
Robert, aliyeibuka katika anga la muziki huo mwaka 2002 na albamu ya Baba.
Katika albamu hiyo Robert ambaye
ana sauti nzito alishirikiana vema na Godwin Gondwe mtangazaji wa ITV ambaye
naye ana sauti ya zege au sauti nzito lakini yenye mvuto sana na kuifanya albamu
hiyo kuwa na mvuto wa kipekee na kuweka imara katika anga la muziki huo.
Albamu hiyo iliyokuwa na nyimbo
kumi iliwashika wengi na kila mpenzi wa nyimbo za injili kupenda kusikiliza
nyimbo zilizokuwemo. Baadhi ya nyimbo zilizokuwamo katika albamu hiyo ni
Baba, Niongoze, Ngulujangu iliyoimbwa kwa kinyakyusa na nyinginezo.
Kufanya vizuri sokoni kwa albamu
hiyo kulikuwa kama kumemtoa kimasomaso Robert kwani mwaka 2003 aliingia
studio na kufyatua albamu ya pili inayojulikana kwa jina la Kiganjani pa
Mungu.
Albamu hiyo ambayo nayo
ilibahatika nayo kufanya vyema katika tasnia ya injili na hivyo ikamlazimu
Robert kurekodi video ambayo nayo ilibamba.
Albamu yake ya tatu ni Adui yangu
ilikuwa na nyimbo nane, hakuna asiyejua kila kitu kinachotengezwa kwa ubora,
hutumia gharama kubwa kukikamilisha.
Hata hivyo Robert alikaa na
kutafari, kwa makini jinsi gani anaweza kurekodi video ambayo inaweza kuwa
tofauti na video zilizotangulia. Jibu lake lilionekana kuwa ni kujiweka sawa
katika fungu la fedha.
Robert aliamua kuzichambua nyimbo
zilizo katika albamu hizo mbili na kufanikiwa kurekodi albamu moja aliyoipa
jina la 'The Best Of David Robert'.
Mwanamuziki huyo anaeleza kuwa
albamu hiyo ilirekodiwa katika mandhari ya kuvutia na mtaalamu wa masuala ya
filamu kutoka nchini Ujerumani Daniel Uphaus kwa kushirikiana na Sye ambaye
ni mtaalamu wa kuongoza filamu.
Wataalamu hao waliirekodi kwa
makini albamu hiyo hali iliyopelekea kukubalika katika soko la kimataifa,
ambapo tayari vituo vya Chanel O na Mtv Base waliiomba kwa ajili ya kuirusha
katika runinga zao.
Ubora wa albamu hiyo ya The Best
of David Robert umetokana na maandalizi ya miaka mitatu aliyoyafanya kabla ya
kuchukua uamuzi wa kuingia studio na kutoa kitu hicho ambacho kinamvuto
mkubwa.
Kukamilika kwa albamu hiyo kulichukua
miezi minne na baada ya kurekodiwa aliipeleka kwa wataalamu wengine kabla ya
kuingia sokoni. Katika kuhakikisha albamu hiyo inakuwa tofauti na albamu
nyingine hasa za muziki wa injili nchini, Robert alisafiri mikoa mbalimbali
kwa ajili ya kupata picha nzuri kutokana na ujumbe wa nyimbo husika.
Mikoa aliyofanikiwa kwenda
kurekodi albamu hiyo ni Morogoro, Iringa, Arusha, Moshi, Pwani na Dar es
Salaam.
Robert aliyezaliwa Machi 18, mwaka
1978 Mabatini, jijini Mbeya anasema kuwa huduma ya uimbaji alianza tangu
akiwa mtoto, alipokuwa shuleni, ambapo aliifanya kwa nguvu zote kwa
kutembelea shule mbalimbali kwa lengo la kutoa injili kwa njia ya nyimbo hiyo
ikiwa mwaka 1998 wakati akisoma Shule ya Sekondari ya Jitegemee, jijini Dar
es Salaam.
Pamoja na kuipenda huduma hiyo
wapo waimbaji waliomvutia akiwamo Mchungaji Ephraim Mwansasu, Mchungaji
Daniel Richard Mwansumbi na Cosmas Chidumule hao ndio waliompa hamasa kubwa
Robert kujikita katika anga la muziki huo wa injili.
Waimbaji hao ndio walikuwa
wakimvutia kutokana na sauti zao kuwa nzuri pamoja na ujumbe wa nyimbo
uliokuwamo ndani ya nyimbo zao na mitindo waliyokuwa wakiitumia.
Kwa upande wa mafanikio kupitia
muziki huo wa Injili Robert anaseama: “Nimefanikiwa kujenga nyumba nzuri ya
kisasa, kumiliki gari lakini mafanikio mengine ni pamoja na kupata mtandao
mzuri wa marafiki ndani na nje ya nchi na kuwa na miradi mbalimbali
inayonisaidia kuendesha maisha yangu ya kila siku,” anasema.
Kwa upande wa changamoto,
mwanamuziki huyo anasema kuwa anakabiliwa na mtaji mdogo wa kuitangaza huduma
ya Mungu ndani na nje ya nchi, kutumia gharama kubwa katika kurekodi albamu
na mwisho wa siku anajikuta mfukoni hana kitu, wapiga picha kuchelewesha
kazi, ambapo kama alikuambia anakupa baada ya wiki mbili basi atakupa baada
ya miezi miwili, masta hazina ubora na teknolojia kuwa chini, isiyokidhi
ubora wa kimataifa na matatizo ya umeme usio wa kudumu pia huchangia kazi
kusuasua.
Anasema kuwa anakerwa sana na
waimbaji wanaokimbilia katika muziki huo kwa kuangalia masilahi ya pesa zaidi
kuliko huduma.
Ambapo watu wengi wamekuwa
wakijikuta wanashindwa kufanya vema kazi ya Mungu pindi wanachokitarajia
kinanapokosekana.
Mwimbaji huyo mwenye mke na mtoto
mmoja anasema wazi bila kificho kuwa muimbaji mwenzake anayetamba na albamu
yake mpya ya ‘Nipe macho’, Christina Shusho, ndiye anayemvutia zaidi kutokana
na nyimbo zake kuwa na ujumbe mzito ambao mara nyingi nyimbo hizo hugusa
maisha anayopitia.
Kwa upande wa matarajio anasema
kuwa anatamani kufanya mapinduzi makubwa katika muziki wa injili kwa siku za
usoni. Mbali na hilo anatamani kuona muziki wa injili ukisambaa kimataifa
zaidi na waimbaji wazalishe kazi zenye ubora wa hali ya juu.
|
No comments:
Post a Comment