Pages

8 May 2014

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA DENGUE (DENGUE FEVER)


 Huyu ndiye mbu aina ya Aides, ambaye ni mweusi mwenye madoadoa meupe yanayong'aa; akikung'ata husababisha kirusi kinacholeta ugonjwa huo.


Utangulizi

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma kuhusu kuendelea kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya dengue hapa nchini. Ugonjwa huu ulithibitishwa kuwepo hapa nchini hususan hapa jijini Dar es Salaam mnamo mwishoni mwa mwezi wa Januari 2014. Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huu kwa kipindi hiki ni 70 ikiwa ni wagonjwa 58 Kinondoni, 7 Temeke na 5 Ilala. Kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita idadi hii ya wagonjwa imeongezeka mara mbili kuliko siku za nyuma. Vilevile kumekuwepo kifo cha mtu mmoja katika hosipitali ya Mwananyamala.

Aidha, ugonjwa huu si mpya hapa nchini kwani uligundulika kwa mara ya kwanza mnamo Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo idadi ya watu waliothibika kuwa na ugonjwa ilikuwa 40, pia kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huu.
Homa ya Dengue

Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes ambao ni weusi na madoadoa meupe yenye kungaa.

Dalili za ugonjwa huu ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususani sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya denge. Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi wanaaswa kuwa wakati wakipata homa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria ua dengue ili hatua stahiki zichukuliwe.
Vilevile mara chache mgonjwa anaweza kutokwa na damu sehemu za fizi, mdomoni, puani, kwenye macho na pia njia ya haja kubwa na ndogo. Dalili hizi za kutokwa damu pia zimeanza kuonekana hapa Dar es Salaam kwa wagonjwa watatu ambapo mmojawapo alipoteza maisha.

Virusi vya homa ya dengue vinaenezwa kwa binadamu baada ya kuumwa na mbu aina ya “Aedes”. Mbu hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba. Viluwiluwi vya mbu hawa huweza kuishi katika mazingara ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu. Mbu hawa huwa na tabia ya kuuma zaidi wakati wa mchana.

Ugonjwa huu hauenezwi kutoka binadamu mmoja kwenda kwa mwingine bila ya kuwepo na kuumwa na mbu mwenye vimelea. Hadi sasa hakuna chanjo ya homa ya denge. Mgonjwa mwenye homa ya dengue anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu. Mgonjwa mwenye dalili za homa ya denge anashauriwa kuwahi mapema kwenye kituo cha kutolea huduma za afya ili kupata huduma stahiki kwani endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu anaweza kupoteza maisha.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue
  • Kuangamiza mazalio ya mbu
  • Fukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo
  • Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
  • Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
  • Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama
  • Funika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara
  • Safisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama
Kujikinga na kuumwa na mbu
  • Tumia dawa za kufukuza mbu “mosquito repellants”
  • Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
  • Tumia vyandarua vyenye viuatilifu (hata kwa wale wanaolala majira ya mchana)
  • Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
Hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa mazalio ya mbu yanaangamizwa na pia kujizuia kuumwa na mbu.

Hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii


• Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara kupitia Makatibu Tawala na Wakurugenzi.

• Ufuatiliaji wa homa hii ulianza kufanyika katika Manispaa ya Kinondoni iliyoonekana kuwa na wagonjwa wengi zaidi ikafuatiwa na Ilala na Temeke. Pia uchunguzi utaendelea katika Mikoa na Wilaya nyingine tukianzia na zile wilaya zitakazoonekana kuwa na ongezeko la wagonjwa wenye homa.

• Kutuma vipeperushi vya ugonjwa huu katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.

• Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya kwenye vituo vya kutolea huduma na mipakani kuhusu namna ya kutambua, matibabu na kujikinga dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa atapatikana.

• Kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa, ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu

• Kutoa elimu kwa waandishi wa habari ili waweze kuisambaza kwa jamii

• Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa dengue uliopo kwenye vituo maalumu ‘Sentinel Surveillance Sites’

• Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara ili kuweza kuthibitisha ugonjwa huu

• Kufanya tathmini ya mazalio ya mbu ili kubaini ukubwa wa tatizo, jamii ya mbu wanaoambukiza ugonjwa, mazingira yao na jinsi ya kuwathibiti

Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu bali wanashauriwa kwenda katika vituo vya tiba mara mnapoona dalili.

Jamii inashauriwa kuhakikisha kuwa mazalio yote ya mbu yanaangamizwa na pia kuzuia kuumbwa na mbu

Vilevile, wizara inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini. Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huu.

Mhe. Dkt. Seif Suleiman Rashid (Mb)
Waziri – Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii
25 Machi 2014

No comments:

Post a Comment