Pages

2 January 2020

JOHN SHABANI NA ZIARA YA KUTEMBELEA BONDE LA OLDUVAI (OLDUPAI)

 Bonde la Olduvai (Oldupai) lililopo nchini Tanzania ni maarufu duniani kutokana na kufahamika kwake kama chimbuko la binadamu wa kale. Historia na umaarufu wa bonde hili unafuatia uvumbuzi wa visukuku vya zamadamu uliofanywa na watafiti Dkt. Louis Leakey na mkewe Dkt. Mary Leakey. Fuvu la binadamu wa kale maarufu kama Zinjanthropus lilivumbuliwa kwenye bonde hili pamoja na visukuku vingi vya wanyama wa kale na masalia mengi ya zana za mawe. Oldupai ipo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, mashariki mwa mbuga za Taifa za Serengeti.

 Tangu utafiti wa mambo ya kale uanze kwenye bonde hili mnamo karne iliyopita, ilidhibitika kwamba teknolojia ya mwanzo kabisa duniani ilianzia hapa kutokana na ushahidi wa zana za mawe za muhula wa kwanza. Ushahidi wa akiolojia na visukuku unaonyesha mabadiliko ya viumbe asilia na maendeleo ya utamaduni wa binadamu wa kale katika nyakati tofauti.

Dhumuni la utafiti mkubwa unaoendelea kwenye bonde la Oldupai ni kuchunguza mabadiliko ya zamadamu na maendeleo ya teknolojia ya zana za mawe kati ya muhula wa mwanzo (Oldowan) na wa pili (Acheulian). Utafiti huu unafanywa na kikundi cha wanasayansi wa kimataifa kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani. Kikundi hiki kijulikanacho kama Olduvai Geochronology and Archaeology Project (OGAP) kinajumuisha wanasayansi kutoka fani mbalimbali za jiolojia, akiolojia, paleontolojia na mazingira.

No comments:

Post a Comment