Nianze kwa kusema, nimekuwa mmoja kati ya waalimu wa sauti na uimbaji, niliyewezesha watu wengi, vikundi vingi, na kwaya nyingi kuimba vizuri.
Lakini pia nashangaa wapo watu wengi wanaokimbilia studio, wanatengenezewa studio lakini ukweli ni kwamba hawajawa waimbaji wazuri, ni waimbaji wa kuimbia CD. Jamani kuimba vizuri kuna gharama zake.
Ikumbukwe kuwa, ili uimbaji wetu au muziki wetu uwe wa viwango vya kimataifa yapo mambo yanayotakiwa kufanyika:
Kwanza ni uandishi mzuri, ubunifu zaidi, studio bora (quality of studio), kuandaa video yenye viwango (quality of video).
Nimekua nikifundisha kwa kina kuhusu hatua nne za kuelekea kuwa na albam bora ya audio, ikiwa ni pamoja na: mwimbaji kuwa bora, tungo bora, muziki bora na studio bora.
Nikualike tena kuhudhuria mafunzo yetu ya sauti yanayoendelea maeneo ya Ukonga. Kwa kuchangia kidogo tu nitakufundisha mbinu za kuwa mwimbaji bora. Tuwasiliane.
Tuendelee na somo:
Unahitaji kufanya nini?
Unahitaji kuboresha sauti yako kwa kupumua vizuri na kutuliza misuli yako badala ya kuiga mtu mwingine.
Kwa Nini Ni Muhimu?
Sauti nzuri hufanya wengine watulie na kufurahia kusikiliza. Sauti mbaya huaribu mawasiliano, na inaweza kumfadhaisha mwimbaji/msemaji na wasikilizaji.
KWA KAWAIDA watu hawavutiwi tu na mambo yanayosemwa, bali wanavutiwa pia na jinsi yanavyosemwa. Ikiwa mtu anayezungumza nawe au anayeimba mbele yako ana sauti nzuri, changamfu, ya kirafiki, na yenye fadhili, utafurahia kumsikiliza kuliko kama ana sauti kali isiyo ya kirafiki, sivyo? Kukuza sifa hizo nzuri hakutegemei tu kuboresha sauti. Kunaweza kuhusu utu wa mtu pia.
Nyakati nyingine sauti isiyofaa inaweza kusababishwa na kasoro fulani ambayo mtu amezaliwa nayo au ugonjwa uliodhuru zoloto. Huenda kasoro hizo zisiweze kurekebishwa katika mfumo huu wa mambo. Lakini, unaweza kuboresha sauti yako ukijifunza kutumia vizuri viungo vya usemi. Kwanza, tufahamu kwamba sauti za watu hutofautiana. Kwa hiyo, usijaribu kuiga sauti ya mtu mwingine. Badala yake, boresha sauti yako mwenyewe pamoja na hali zake. Unawezaje kufaulu? Kuna mambo mawili makuu. Pumua Vizuri. Ili sauti yako iwe nzuri, unahitaji hewa ya kutosha na unahitaji kupumua vizuri. Bila kufanya hivyo, sauti yako inaweza kuwa dhaifu mno na unaweza kukata-kata maneno katika hotuba yako.
Sehemu kubwa za mapafu haziko juu kifuani; sehemu hizo huonekana kubwa kwa sababu tu ya mifupa ya mabega. Lakini, sehemu za mapafu zilizo pana zaidi ziko chini, juu tu ya kiwambo. Kiwambo kinashikana na mbavu za chini na kinatenganisha kifua na tumbo.
Ukivuta pumzi na kujaza tu sehemu za juu za mapafu, utakosa pumzi haraka. Sauti yako itakosa nguvu na utachoka haraka. Ili uvute pumzi vizuri, unahitaji kuketi au kusimama vizuri na kurejesha mabega nyuma. Jaribu sana usipanue sehemu ya juu pekee ya kifua unapovuta pumzi. Kwanza vuta pumzi kabisa. Sehemu za chini za mapafu zikijaa hewa, mbavu zako za chini zitapanuka. Kwa wakati huohuo, kiwambo kitasonga chini, kikisukuma chini kwa utaratibu sehemu za tumbo hivi kwamba utasikia mkazo kwenye mshipi wako au kwenye vazi katika eneo la tumbo. Lakini mapafu hayako kwenye eneo la tumbo; yamefunikwa na mbavu. Unaweza kuthibitisha jambo hilo kwa kuweka mkono mmoja kila upande wa mbavu za chini. Kisha vuta pumzi kabisa. Kama unavuta pumzi vizuri, utaona kwamba huingizi hewa tumboni na kuinua mabega. La, badala yake, utasikia mbavu zikisonga juu kidogo na kupanuka.
Kisha, jaribu kushusha pumzi. Usishushe pumzi kwa ghafula. Ishushe polepole. Usijaribu kuzuia pumzi kwa kukaza koo kwa sababu sauti itajikaza au itakuwa nyembamba sana. Mkazo wa misuli ya tumbo na mkazo wa misuli iliyo kati ya mbavu huondosha pumzi, lakini kiwambo hudhibiti mwendo wa pumzi hiyo.
Msemaji anaweza kudhibiti jinsi anavyopumua kwa kujizoeza kama vile tu mwanariadha anavyofanya mazoezi ya mbio. Simama vizuri kama umerejesha nyuma mabega, vuta pumzi kabisa ili sehemu za chini za mapafu zijae hewa, kisha shusha pumzi polepole na kwa utaratibu ukihesabu kwa kadiri uwezavyo kabla ya kuvuta tena pumzi. Kisha jizoeze kusoma kwa sauti ukipumua kwa njia hiyo.
Tuliza Mkazo wa Misuli. Jambo jingine muhimu linalotokeza sauti nzuri ni utulivu! Unaweza kuboresha sana sauti yako ukijifunza kutulia unapozungumza. Ni lazima akili na mwili zitulie, kwa kuwa mkazo wa akili husababisha mkazo wa misuli.
Ifikirie misuli ya koo na kujaribu kuituliza. Kumbuka kwamba nyuzi zako za sauti hutikisika zinapopitisha hewa. Sauti hubadilika misuli hiyo ikikazika au ikitulia kama tu vile uzi wa gitaa hubadili sauti ukikazwa au ukilegezwa. Sauti hurudi chini nyuzi za sauti zinapotulia. Kutuliza misuli ya koo pia hufanya mianzi ya pua ibaki wazi, na hiyo huboresha sauti.
Tuliza mwili wako mzima—magoti, mikono, mabega, na shingo. Ukifanya hivyo, utaweza kuvumisha sauti vizuri ili isikike wazi. Sauti huvumishwa wakati mwili wote unapohusika kuitokeza, lakini mkazo huizuia. Sauti hutokezwa kwenye zoloto nayo huvumishwa katika mianzi ya pua, kwenye mifupa ya kifua, meno, na kaakaa ya mdomo na mianya iliyo katika mifupa ya pua. Sehemu hizo zote zinaweza kuchangia ubora wa sauti. Ukiweka kitu kwenye kibao cha gitaa cha kupaazia sauti, sauti itafifia; ni lazima kibao hicho kisiwe na kitu ili kitikisike na kutoa sauti vizuri. Ndivyo ilivyo pia na mifupa ya mwili wetu ambayo imeshikiliwa na misuli. Uvumishaji mzuri wa sauti unakuwezesha kuwa na ubadilifu wa sauti na kuweza kuonyesha hisia mbalimbali unapoimba au kuzungumza. Pia utaweza kuimbia au kuhutubia watu wengi zaidi bila kukaza sauti.
JINSI YA KUFAULU
Fanya mazoezi ya kuvuta pumzi, ukijaza sehemu za chini za mapafu kwa hewa.
Unapozungumza, tuliza misuli yako ya koo, shingo, mabega, na mwili wote mzima.
MAZOEZI: (1) Kwa dakika chache kila siku katika juma, fanya mazoezi ya kuvuta pumzi kabisa mpaka uzijaze sehemu za chini za mapafu yako. (2) Jaribu kutuliza misuli ya koo unapoongea, angalau mara moja kwa siku.
SAUTI HUTOKEZWAJE?
Sauti zote hutokezwa na hewa inayotoka mapafuni. Mapafu hupiga hewa kama pampu kupitia koo na kuingia ndani ya zoloto ambayo iko katikati ya koo. Ndani ya zoloto mna misuli miwili midogo inayoitwa nyuzi za sauti, msuli mmoja uko upande mmoja na msuli mwingine upande mwingine. Nyuzi hizo za sauti ndizo vitokezaji vikuu vya sauti. Misuli hiyo hufungua na kufunga njia ya hewa katika zoloto ili kuingiza hewa na kuitoa na vilevile kuzuia vitu visivyotakikana visiingie kwenye mapafu. Tunapopumua kwa njia ya kawaida nyuzi za sauti hazitokezi sauti wakati hewa inapopita. Lakini mtu akitaka kuimba au kuzungumza, misuli hufinya nyuzi za sauti, na nyuzi hizo hutikisika wakati hewa inayotoka mapafuni inaposukumwa kuzipitia. Utaratibu huo hutokeza sauti.
Kadiri nyuzi za sauti zinavyokazika, ndivyo zinavyotikisika kwa kasi zaidi na ndivyo sauti inavyoinuka. Na kadiri nyuzi hizo zinavyolegea, ndivyo sauti inavyopungua. Mawimbi ya sauti yanayotoka kwenye zoloto huingia sehemu ya juu ya koo inayoitwa koromeo. Kisha mawimbi hayo hupitia mdomo na pua. Hapo sauti nyinginezo huongezwa ili kurekebisha, kukuza, na kuimarisha sauti ya awali. Kaakaa la mdomo, ulimi, meno, utaya, na midomo huungana pamoja ili kutawanya mawimbi ya sauti, na kutokeza usemi unaoeleweka.
Sauti ya mwanadamu ni ajabu sana, na haina kifani ikilinganishwa na chombo chochote kile ambacho binadamu ametengeneza. Ina uwezo wa kuonyesha hisia mbalimbali kama vile upendo na chuki kali. Sauti ikikuzwa na kuzoezwa vizuri, inaweza kubadilikana sana na kutokeza nyimbo tamutamu na semi zinazogusa mioyo.
KUSHINDA MATATIZO FULANI HUSUSA
Sauti dhaifu. Sauti ndogo huenda isiwe dhaifu. Ikiwa nzuri na yenye kuvutia, wengine wanaweza kufurahi kuisikiliza. Lakini ni lazima sauti iwe yenye kiasi kinachofaa ili iweze kufaidi wengine.
Ili uboreshe ukubwa wa sauti yako, unahitaji kuivumisha zaidi. Unahitaji kutuliza mwili wote mzima, kama ilivyoonyeshwa katika somo hili. Pamoja na kutuliza mwili, fanya mazoezi ya kuimba hali umefunga midomo. Midomo inapaswa kugusana kidogo, isishikane sana. Unapoimba kwa njia hiyo, sikia mitikisiko ya wimbo huo akilini na kifuani. Nyakati nyingine sauti husikika kuwa dhaifu au kukazika kwa sababu ya ugonjwa au kukosa usingizi. Bila shaka, hali hiyo ikiboreka, sauti itaboreka.
Sauti inayoinuka juu sana. Mkazo kwenye nyuzi za sauti hufanya sauti iinuke. Sauti yenye mkazo hufanya wasikilizaji wawe na mkazo. Unaweza kupunguza sauti nyembamba kwa kutuliza misuli ya koo ili kupunguza mkazo kwenye nyuzi za sauti. Jaribu kufanya hivyo, ukifanya mazoezi kila siku unapozungumza. Pia ni vizuri kuvuta pumzi kabisa.
Sauti ya kubana pua. Nyakati nyingine pua iliyofungika hutokeza tatizo hilo, lakini mara nyingi hali hiyo husababishwa na jambo jingine. Nyakati nyingine kwa kukaza misuli ya koo na mdomo, mtu hufunga mianya ya pua na kuzuia hewa isipite vizuri. Jambo hilo hutokeza sauti inayobana pua. Unahitaji kutulia ili kuepuka jambo hilo.
Sauti nzito na kali. Sauti kama hiyo haitokezi mazungumzo ya kirafiki. Inaweza kutisha wengine. Katika hali fulani, jambo muhimu ni kuendelea kujitahidi kubadili utu wako. Ikiwa tayari umefanya hivyo, kujaribu kutumia kanuni za kurekebisha sauti kunaweza kusaidia. Tuliza koo na taya. Kufanya hivyo kutafanya sauti yako ipendeze zaidi na kufanya maneno mengine yasitokee vibaya kwa kuyalazimisha kupitia meno.
Karibu katika darasa la sauti, ili ufanyike kuwa mwimbaji, muhubiri, msemaji bora. Kumbuka, sauti yako ndio wewe!
John Shabani
0 comments:
Post a Comment