5 March 2017

HUU NDIO UWEKEZAJI UNAOLIPA KULIKO UWEKEZAJI MWINGINE





Kuna uwekezaji mmoja unaolipa kuliko uwekezaji mwingine wowote. Ukiwekeza vizuri kwenye uwekezaji huu, lazima uwekezaji mwingine utalipa tu. Ukishindwa kuwekeza vizuri kwenye uwekezaji huu, hautafika mbali kwenye safari ya mafanikio.

Kuna uwekezaji mmoja unaolipa kuliko uwekezaji mwingine wowote. Ukiwekeza vizuri kwenye uwekezaji huu, lazima uwekezaji mwingine utalipa tu. Ukishindwa kuwekeza vizuri kwenye uwekezaji huu, hautafika mbali kwenye safari ya mafanikio.

Uwekezaji huu ni kuwekeza kwako wewe binafsi. Ni kujitengeneza wewe binafsi. Kuitengeneza akili yako, mwili wako, roho yako, hisia na mahusiano yako na wengine. Ili uwe na mafanikio makubwa lazima uwekeze kwako binafsi kwanza.
Kuna maeneo manne ambayo unahitaji kuyafanyia kazi kila siku ili uwe na ufanisi mkubwa kwenye yale unayofanya. Haya hapa ni maeneo makuu manne unayotakiwa kuwekeza;
- Eneo la kwanza ni afya ya kiroho au imani.
Hili ni eneo lenye umuhimu sana kwako na ni eneo linalokupa maana halisi ya maisha yako. Kila siku ni lazima ukue kiroho, kila siku ni lazima uhakikishe unakua imani yako. Kila siku unahitaji kujenga imani yako, ili maisha yako yawe na maana. Kila siku hakikisha unaungana na chanzo chako cha kiroho (kwa maombi, sala au tajuhudi (meditation)) na kuwa mtu wa kushukuru kwa kila jambo.
- Eneo la pili ni mwili.
Bila kuwa na afya bora ya mwili wako, ni ngumu sana kutekeleza majukumu mengine kwenye maisha yako. Kama mwili wako unasumbua hata mafanikio yako huwezi kabisa kuyafurahia.
Ni lazima utunze sana mwili wako. Hakikisha unakula chakula bora na kufanya mazoezi ili kuujenga mwili wako. Pata muda wa kutosha wa kupumzika pia. Usingangane kutafuta mafanikio kwa kujitesa sana mwili wako. Hakuna maana ya kupata mafanikio, alafu mwisho wa siku unakuwa mgonjwa na unashindwa kufurahia mafanikio yako. Wekeza kwa kutunza mwili wako.
- Eneo la tatu ni akili.
Ili uwe na ufanisi mkubwa, unahitaji kutunza afya yako ya akili. Afya yako ya akili inatunzwa kwa kuongeza maarifa kila siku. Soma vitabu, kati ya vitabu vizuri vya kuvisoma ni pamoja na kile nilichokiandika mimi mwenyewe, kitafute au toa oda nitakutumia. Kinaitwa "MARUFUKU KUKATA TAMAA". sikiliza kanda za sauti kukuhamsisha na kukufundisha, hudhuria semina na kuna muda inabidi urudi darasani kusoma. Kuandika pia ni njia nzuri ya kuwekeza kwenye akili yako, kuwa na sehemu ya kuandika kila siku. Kuandika kunaifanya akili yako ifikiri vizuri.
Je Unailisha Nafsi Yako Kama Unavyoulisha Mwili Wako?
Watu wengi tunakula mara tatu kwa siku yaani kifungua kinywa, chakula cha mchana na chakula cha usiku. Ukweli tunahitaji chakula bora ili mili yetu iweze kufanya kazi. Mili yetu inapokuwa na njaa, ni sharti kuipa chakula.
Kwenye kuipa mili yetu chakula uwa hatuko nje ya muda. Tumekuwa ni wazuri sana kufata ratiba yetu ya kula, inapofika muda fulani tunajua kabisa tunatakiwa kula, kwa hiyo tunatafuta chakula tunakula.
Mili yetu tunaijali sana, lakini nataka nikuulize swali moja; je unailisha nafsi yako kama unavyoulisha mwili wako? Ukweli watu wengi hatuzilishi nafsi zetu chakula. Rafiki kama unakula mara tatu kwa siku, je ni mara ngapi kwa siku unailisha akili yako?
Inawezekana unatumia zaidi ya elfu kumi kwa siku kwa ajili ya chakula cha mwili. Je unatumia shilingi ngapi kwa siku kwa ajili ya chakula cha nafsi yako?
Rafiki, naamini ulishawai kusikia mtu anasema kuliko kupoteza shilingi elfu tano kwa ajili ya kitabu ni bora hiyo pesa niende nikale chakula. Hili limenitokea mara nyingi ninapohamasisha watu kununua kitabu changu. Watu wengine kununua kitabu kwa ajili ya nafsi yake ni kupoteza pesa, anaona kama anaibiwa vile. Naamini sio wewe rafiki.
Watu wengi waliofanikiwa uwa tunaona kama ni wenye bahati tu. Lakini ukifatilia unakuja kujua watu hawa hawajafanikiwa kwa bahati tu. Moja ya kitu ambacho wanakifanya kila siku na kinawafanya wazidi kufanikiwa ni kuzilisha nafsi zao. Yaani kila siku lazima aingize kitu kipya kwenye nafsi yake.
Punguza muda mwingi unaoperuzi kwenye mitandao ya kijamii, kusikiliza redio na kuangalaia Tv. Na tumia muda huo kuwekeza kwenye akili yako. Usipokuwa makini na mambo unayoingiza kwenye akili yako, dunia itakuendesha.
- Eneo la mwisho ni hisia na mahusiano.
Hapa unahitaji kuhakikisha mahusino yako na hisia zako zinaenda sawa. Unapojenga mahusiano bora, yanajenga hisia bora pia. Hakikisha unaboresha mahusiano yako na watu wako wa karibu na watu wengine wanaokuzunguka. Hakuna maana ya kubanana na mafanikio, ukakosa muda wa kutosha wa kuwa na familia yako na watu wako wa karibu. Hakikisha unapata muda wa kutosha wa kuwa na watu wako karibu. Hii itajenga hisia zako.
Mambo Mawili (2) Yanayojenga Mahusiano Bora:
Kwa sababu mahusiano yetu yana mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yetu, leo naomba tujifunze/ tujikumbushe mambo mawili ambayo yatatusaidia kujenga mahusiano bora kati yetu na watu wengine. Haya hapa ni mambo mawili yanayojenga mahusiano yetu:
Upendo
Bila upendo mahusiano yetu lazima yatapoa. Bila upendo mahusiano yetu na wengine yanapoteza thamani. Ni wajibu wako rafiki yangu kuwapenda wengine kama unavyojipenda wewe. Ipende familia yako, mpende bosi wako, wapende wafanyakazi wenzako, wapende wateja wako, wapende wafanyabiashara wenzako.
Kama binadamu kila mtu ana mapungufu yake. Kama binadamu kuna kipindi tunakosea. Upendo unapokuwepo ni rahisi sana kwa watu kusameheana pale wapokoseana. Upendo unapokuwepo unaficha madhaifu yetu pia na kutufanya tuishi kwa furaha na amani na watu wengine.
Upendo unawafanya watu wawe karibu zaidi. Kinyume cha upendo ni chuki. Chuki inabomoa, upendo unajenga. Chuki inaleta kugombona, upendo unapatanisha. Ili tufanikiwe tunahitaji kupendana bila kuangalia dini zetu, kabila zetu, hata rangi zetu. Tumeumbwa na Mungu kwa kutegemeana ni jukumu letu kupendana na sio kubaguana.
Kuheshimiana
Tunapaswa kuwaheshimu wengine. Mme muheshimu mke na mke muheshimu mme. Watoto wawaheshimu wazazi na wazazi wawaheshimu wanao. Kila mtu anapenda kuheshimiwa, kila mtu anapenda kuona anapewa heshima kwa vile alivyo na kwa mchango anaotoa.
Hayo ndio maeneo manne makubwa unayohitaji kuwekeza. Huu ni uwekezaji unaolipa kuliko uwekeza mwingine wowote. Ukiwekeza vizuri, matunda yake sio haba na hii itajenga sana ufanisi wako.
Tafakari njema rafiki yangu. Tuko pamoja.

0 comments:

HEART OF WORSHIP

HEART OF WORSHIP