21 June 2015

MAADHIMISHO YA SIKU YA WAJANE DUNIANI TAASISI YA RITA KUTOA DARASA KWA JAMII KUHUSU KUFAHAMU KUHUSU UANDISHI WA WOSIA NA FAIDA ZAKE





 Wananchi mbalimbali wakiwa wamejitokeza kwa wingi katika banda la rita, wakijifunza mabo mbalimbali hasa yale yahusuyo kuandika wosia na, vyeti vya kuzaliwa na sheria mbalimbali


Labda nikudikeze darasa kwa kwa ufupi

WOSIA

1.  Wosia ni nini?

Wosia ni tamko analotoa mtu wakati  wa uhai wake akieleza jinsi anavyotaka mali yake igawanywe au wapewe watu gani  baada ya kifo chake.

2.  Nani anaweza kuandika wosia?

Ni mtu yeyote mwenye umri wa miaka 18 au zaidi  na mwenye akili timamu.

3.  Faida za wosia.

-         Kuepusha  watoto au mke/mume  kunyang’anywa mali.
-         Kuepusha  migongano katika  familia, ndugu au jamaa zake.
-         Kuepuka kumrithisha mtu yeyote ambaye kisheria hapaswi kurithi mali yako.
- Unakupa uhakika wa maisha bora ya baadae ya warithi wako kulingana na mali ulizo nazo
- Kupunguza gharama/usumbufu wakati wa kuendesha mirathi.


4.  Sababu za kuandika  wosia

-         Kuweka msimamizi wa mirathi  na mlezi wa watoto  wako au mwangalizi wa familia.
-         Kutoa maelekezo kuhusu  mali zako  kama  upendavyo na kwa kufuata sheria.

5.   Wosia unaokubalika kisheria

-         Uwe na wa maandishi au matamshi

-         Ushuhudiwe na watu wawili ikiwa ni wa maandishi.
-         Ushuhudiwe na watu wa nne ikiwa ni  wa matamshi.
-         Uwe wosia usiomnyima mrithi halali mali bila sababu zinazotambulika kisheria.

6.  Ni nani mrithi halali kisheria?

-         Mke au mume
-         Watoto waliozaliwa ndani ya ndoa
-         Watoto waliohalalishwa  kisheria
-         Wazazi na ndugu wa karibu ambao walikuwa tegemezi kwa mtoa wosia wakati wa uhai wake.

7.  Hali ya mwandika wosia

Anayeandika wosia ni lazima athibitishwe kuwa ana akili  timamu wakati akiandika au kutamka wosia wake.

8.  Mambo muhimu ya kuzingatia katika  kuandika wosia.

·        Majina ya wanaonufaishwa
·        Orodha ya mali za mtoa wosia  na mahali zilipo na stakabathi / hati za ununuzi  / Umiliki wa mali hizo.
·        Majina na anuani za msimamizi wa  mirathi na mwangalizi  wa watoto
·        Maelezo mengine ya kuweka kwenye wosia.

9.  Ni wapi wosia uhifadhiwe?

-         Wosia uhifadhiwe mahali ulipoandaliwa.
-         Kwenye taasisi za dini kama vile kanisa au msikiti.
-         Kwa mwanasheria yeyote
-         Kwa mtu yeyote asiyemrithi katika wosia husika na awe na sifa za kuaminika za kutunza siri.
                 
 Hayo ni machache tu kati ya mengi ambayo yatafundishwa katika viwanja vya mnazi mmoja Dar es salaam, jumanne ya tarehe 23 Juni 2015
Watu wote mnakaribishwa.


MENGINEYO

KWA watu wengi wa jamii za Kiafrika, mtu kuandika au kutoa wosia juu ya mali zake, ni kitu ambacho inachodhaniwa ni mkosi..., Pia hudhani kwamba anayeandika wosia ni mtu anayejichulia au kujitabiria kifo cha karibu!

Ukweli ni kwamba, wosia ni mojawapo ya vitu vinavyosaidia kuilinda familia na jamii inapotokea mtu aliyeandika wosia huo amefariki dunia. Wakati fulani, uandishi wa talaka unasaidia sana kusaidia usuluhishi wa matatizo ya kifamilia kuhusu mali na fedha za marehemu pindi kifo cha mtu aliye na mali akifariki dunia .
Kwa mujibu wa kifungu cha 2 cha sheria ya Usimamizi wa Mirathi ya Tanzania, wosia ni tamko la mwisho la mtu anayetoa tamko hilo, akielezea jinsi gani mali zake zitunzwe au kufanyiwa kazi pindi atakapofariki dunia. Kwa ajili hiyo, mtu aliyetoa tamko hilo, anatakiwa kutoa tamko ambalo ni la mwisho katika matamko yote aliyowahi kuyatoa wakati wa maisha yake juu ya mali na fedha zake zinapaswa kufanywa pindi atakapofariki dunia. Wosia unaweza kuwa wa maneno ya mdomo na vilevile wosia unaweza kuwa wosia uliondikwa kwa maandishi. Kati hali yoyote ile, wosia wa mdomo na wosia wa maandishi unakuwa na nguvu sawa kisheria, ili mradi tu masharti yanayopaswa kuzingatiwa yakitimizwa.

Hata hivyo, kwa wosia wa maandishi au ule wa mdomo, kuna masharti kadhaa yanayohitajika kutimizwa kwa wosia huo kuwa na nguvu kisheria. Mtu anayeandika wosia kimsingi anatakiwa kuwa na mali anayoimiliki yeye binafsi (si ya anayoimiliki kwa ubia au aliyopewa kutokana na wadhifa wake labda kiserikali au kampuni). Vilevile wosia lazima uoneshe nia ya mtamkaji kuhusu kutoa mali zake (pamoja na fedha) kwa watu au mtu fulani na vilevile ndugu msomaji unatakiwa ujue kwamba wosia utakuwa na nguvu kisheria pale tu ambapo mwandishi/mtoa wosia huo atakapokuwa amefariki dunia.
Kwa wosia wa mdomo mpaka uwe una nguvu kisheria, ni lazima ushuhudiwe na watu au kwa maneno mengine mashahidi wasiopungua wanne na kati ya hao, wawili ni lazima wawe watu kutoka katika ukoo wake. Hali hii si tofauti sana kwa upande wa wosia unaoandikwa kwa maandishi, kwani wosia huu ni lazima ushuhudiwe na watu wasiopungua wawili na kati ya hao mmoja ni lazima awe ni mtu kutoka katika ukoo wa mtoa wosia. Hawa wanaweza kuwa wajomba, mashangazi, kaka au dada wa mtoa tamko la wosia.

Zaidi ya hayo, wosia hauwezi kuwa na athari yoyote kisheria kama mtoa tamko la wosia hatatia saini yake aidha kwa maandishi au kwa kuweka dole gumba katika karatasi yake ya wosia. Hii ina maana kwamba mahakama haitautambua wosia huo kama hautakuwa na sahihi ya mtoaji wa tamko hilo. Hata hivyo, wosia hata kama utakuwa na vigezo vyote vinavyotakiwa lakini kama mtoaji wake alitoa tamko lake akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa akili au kulazimishwa/kushurutishwa, hii ni mojawapo ya vigezo vya kukataa kuidhinisha wosia au mirathi kwa mtu yeyote na mahakama. Wosia vilevile ni lazima umtaje mtu atakayeutekeleza. Huyu ni mtu ambaye mtoa wosia atamchagua katika wosia wake na ndiye atakayepewa majukumu yote ya kuangalia jinsi gani matakwa ya mtoa wosia yatavyotimizwa. Ni kweli kwamba mtu anaweza kuandika wosia na kuufuta wakati wowote na mara zote anazotaka. Sheria haina pingamizi juu ya jambo hilo.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba mtoa wosia anaweza kubadilisha mawazo yake wakati wowote ule. Hata hivyo, wakati wowote mtu atakapokuwa anaandika wosia, ni lazima aandike kwamba wosia huo ni wa mwisho kabisa kati ya wosia mwingine aliowahi kuuandika. Hata hivyo, mahakama imepewa uwezo kisheria kutengua au kubatilisha wosia wowote kama haukidhi vigezo vya kisheria kuufanya uwe halali. Katika hali kama hii, familia itatakiwa kumchagua mtu asimamie mirathi kana kwamba marehemu hakuacha wosia wowote kwani wosia wake hautakuwa na nguvu yoyote kisheria. Ikiwa baada ya kifo cha mtu aliyeandika wosia, kutakutwa wosia mbili tofauti na ulioandikwa siku na tarehe tofauti, basi wosia wa tarehe ya mbele ndio utahesabika kuwa halali na si wa tarahe ya nyuma yake. Hapa sheria inatumia busara kwamba mpaka wosia mwingine uandikwe ina maana marehemu alibadili mawazo yake na ndiyo maana akaandika wosia mwingine.

Wosia unapata nguvu kisheria pale tu aliyeandika akifariki dunia. Hii ina maana kwamba, hata kama mathalani, mtoto wa marehemu ndiye aliyeandikwa atarithi shamba la marehemu, mtoto huyo hatakuwa mmiliki halali wakati mwandishi wa wosia huo atakapokuwa hai, ila tu pale atakapofariki dunia ndipo mtoto huyo ataweza kuwa mmiliki halali wa shamba hilo. Kimsingi, ni haki ya mwandika au mtoa wosia kubadilisha wosia wake wakati wowote autakao. Vilevile ni haki yake kumpa urithi mtu yeyote atakayekuwa amemchagua katika wosia wake. Hata hivyo, mwandishi wa wosia ni lazima azingatie watoto ambao ni wategemezi kwake pale atakapokuwa anaandika/anapotoa wosia wake.
Unafahamu masharti ya Wosia...?
- Mtoa wosia lazima awe na akili timamu.
- Awe ametimiza miaka kumi na nane (18) na kuendelea.
- Uonyeshe tarehe ,mwezi na mwaka ulioandikwa.
- Uonyeshe majina ya warithi.
- Mtoa wosia ahusishe mali zake binafsi na si za mtu mwingine.
- Wosia ni siri wanufaika hawatakiwi kuujua.
- Mtoa wosia lazima aweke saini yake, na kama hajui kusoma na kuandika aweke alama ya dole gumba la mkono wa kulia.
- Mashuhuda lazima waweke saini zao tena kwa wakati mmoja.

0 comments:

HEART OF WORSHIP

HEART OF WORSHIP