13 September 2015

NGUVU YA KUSIFU NA KUABUDU

NGUVU YA KUSIFU NA KUABUDU
              John Shabani
 
Baada ya kukamilisha kitabu "MARUFUKU KUKATA TAMAA" Sasa niko mbioni kukuletea kitabu kipya kiitwacho "NGUVU YA KUSIFU NA KUABUDU". Najua umesoma vitabu vingi vinavyohusu habari ya kusifu na kuabudu, lakini mimi nakuhakikishia, kitabu hiki kitakusaidi sana. Lakini pia utaelewa tofauti iliyopo kati ya kusifu, kuabudu na kutumika, na zaidi utaimarika sana.

Pamoja na kwamba bado kinaendelea kuhaririwa, lakini acha nikupe utangulizi:


Somo la Kusifu, kumwabudu Mungu ni moja ya masomo muhimu na la kupewa kipaumbele cha kwanza katika kanisa. Lakini pia ni mojawapo ya somo lililosahauliwa hasa katika kizazi hiki, japo katika miaka ya karibuni Mungu amekuwa akirejeza huduma hii kwa watu wake.
Tangu mwanzo Mungu alipomuumba mwanadamu, lengo kuu la Mungu ni kwamba mwanadamu amwabudu na kumtumikia. Hii ni sababu kuu ya Mungu kumuumba mwanadamu tafauti na kiumbe chochote. Mungu wetu anahitaji kuwa na ushirika na mwanadamu, ibada ni njia pekee na kuu ya kuwa na ushirika na Mungu. Wapo wanaoabudu hawataki kutumika pia wanaotumika hawaabudu. Katika kitabu cha kutoka sura 20: 16, hii ni sehemu ya maandiko yaliyoandikwa na Mungu mwenyewe tofauti maandiko mengine yalioandikwa na waandishi 40 walioandika Biblia. Sehemu hiyo ni amri, hivyo si ombi, ni lazima kumwabudu Mungu na kumtumikia Yeye peke yake.
Ukweli ni kwamba, wakristo wameitwa kuabudu. Bwana anahitaji hilo kwanza kabla ya kitu kingine chochote, Ndio sababu za kuandika kitabu hiki ili kuwasaidia wakristo na kila mwenye pumzi ya uhai, afahamu au kuelewa umuhimu wa kumwabudu Mungu.
Kama lilivyo jina la kitabu hiki “Nguvu ya kusifu na kuabudu” Ni ukweli usiopingika kwamba kusifu na kuabudu kunamfanya Mungu akutembelee katika hali zako na kuleta mabadiliko sawa sawa na uweza wake na mapenzi yake. Mimi nimeona nguvu hii na nimeionja. Ninaposifu mambo mengi sana yanafanywa upya ndani yangu na hata mazingira yanayonizunguka. Hiyo ndio nguvu ya kusifu na kuabudu katika roho na kweli, hakuna kitakachobaki jinsi kilivyo maana Mzee wa siku akishuka yote yanabadilika. Hiyo ndio nguvu iliyo katika sifa. Wewe huoni hata ukimsifia mtu wa kawaida utaona hata hali mwitikio wa mtu huyo. Wakati mwingine tumepewa kile tulichokuwa tunakihitaji kwa watu fulani baada tu ya kutanguliza sifa fulani. Hujui kwanini? Sifa ina nguvu na ndio maana Mungu hataki kushirikiana sifa zake na watu wala utukufu wake hatampa mwingine.

Fahamu kuwa uwepo wa Mungu unaleta amani, furaha, pumziko, unawavuta na kuvutia watu sahihi, unaleta baraka, unaleta nguvu, unaleta hekima heshima, uponyaji wa kiroho na kimwili, maono na ufunuo. Kwa kifupi kabisa uwepo wa Mungu kwetu ni suluhisho na majibu ya mahitaji yetu yote hapa duniani sasa na hata milele. kumbuka tutakuwa naye uso kwa uso milele na milele yote maana yeye ndiye ukamilifu wetu. Najua utajiuliza, kwanini kwa wakati mmoja ninachanganya kusifu, kuabudu na kutumika! Huu ni utangulizi tu, kadri utapoendelea kuzisoma kurasazingine, ndipo utakapo elewa zaidi.

Yesu aliwaambia wazi wanafunzi wake kwamba Baba anawatafuta waabuduo “… Baba anawatafuta watu kama hao wamwabudu”. (Yohana 4 : 23). Kumbuka, Baba hatafuti ibada bali watu wanaoabudu. Kuabudu ndio wito wetu wa kwanza tafauti na watu wengine wanavyodhani kwamba hoja kuu ya Mungu ni ya watendaji, hii si kweli. Waabuduo wa kweli mara nyingi huwa watenda kazi au watumishi wa kweli. Yesu pamoja na shughuli nyingi alizokuwa nazo, Biblia inasema alikuwa hana budi kupita katikati ya samaria japo safari yake ilikua ya kwenda Galilaya, ili tu kumsaidia mtu mmoja kuhusu uhalisi wa kuabudu (Yn 4.3-4) tafsiri ya King James katika mstari huo wa nne inasema “And He must needs go through Samaria”, ikimaanisha kuwamba, kulikuwa na uhitaji wa Yesu kulazimika kupitia samaria. Tafsiri ya kisasa ya Amplified Bible inasema “It was necessary for Him to go through samaria” ikimaanisha kulikuwa na umuhimu wa Yesu kufika samaria. Kama nilivyotanulia kusea, tukiwa na waabuduo halisi, hatutapata shida ya watenda kazi wazuri, hivyo Yesu alijua fika kwamba mtu huyo mmoja akibadilishwa ataweza kubadilisha maelfu ya watu.
(Yohana 4:19-24) Historia ya mwanamke huyu, yeye hakuwa myaudi, alikuwa mtaifa. Upatikanaji wa maji wakati huo ulikua mgumu, watu walijenga desturi ya kuchota maji asubui sana. Lakini ilikuwa ni vigimu kwa mwanamke huyu kuamkia kuchota maji kulingana mfumo wa maisha yake ya uovu, alikuwa ni mtu wa kusutwa, alikua mwizi wa waume za watu. Mpaka anakutana na Yesu alikua na wanaume watano. Mwanamke huyu alifahamu fika kuhusu historia ya kuabudu kwa kidini, kuabudu kusikokuwa na hofu ya Mungu. Ndio maana sasa anamwambia Yesu kuwa baba zao waliabudu katika mlima huu ingawa wayahudi waliwaambia wanatakiwa kwenda kuabudu Yerusalemu maana ndiko mahali kuwapasako kuabudia. Yule mwanamke alimuuliza Yesu swali la siku nyingi juu ya mahali panapofaa kwa ibada. Elewa kwamba, kwa karne saba Wayaudi na Wasamaria wamekuwa wakibishana juu ya swala hilohilo, juu ya mahali panapofaa kwa ibada.Yesu hakumbishia mwanamke yule, maana aliyaelewa hayo. Hapa Yesu anasema kwamba mahali hapakuwa na maana sana, cha muhimu ni hali ya moyo wa kila mtu, na jinsi anavyomheshimu Mungu. Hayo ndiyo yanaamua jinsi ibada yake ilivyo. Lakini akamwonyesha na kumfundisha kwa usahihi juu ya hilo. Jambo la ajabu lililo mtokea mama yule baada ya kuelewa ukweli na kumjua mtu anayeongea naye kuwa si mkuu wa dini fulani, sio mtu wa kawaida; Kwanza kiu yake ya uovu ilikatika maana aliyapata maji yaliyo hai. Pili alitubu dhambi zake, maisha yake yakabadilishwa kabisa. Tatu mfumo wake wa ibada ulibadilishwa kabisa maana alifundishwa uhalisia wa kuabdu, aliabudu sasa katika roho na kweli, na baada ya hapo ndipo nne, bila kusukumwa, kusukwasukwa, kuhimizwa wala kubembelezwa, akamtumikia Mungu, akawa mtenda kazi mzuri. Hakika utumishi ukajitokeza ghafla (Yohana 4:28). Hakika huwezi ukawa mwabudu mzuri na usitumike. Katika kizazi tulichonacho mifumo yetu ya ibada imebadilika kabisa, tumeabudu kidini, tuna hitaji kuujua ukweli huu utakao tufanya tubadilishwe kabisa na tuwe waabuduo halisi. Mazingira ya kumwabudu ni muhimu sana yakaeleweka kwa uzuri. Napenda niseme hapa kuwa mahali popote panafaa kumwabudu Mungu, Kwanini? kwasababu Mungu ni Roho na wote wanaotaka kumwabudu imewapasa kumwabudu yeye katika hali hiyo hiyo, yaani katika roho na kweli. Fahamu kuwa roho yoyote haifungwi na mazingira. Kuabudu katika Roho inamaana kuabudu ukiongozwa na Roho. Tukijua ukweli huu na kuufanyia kazi, hakutakuwa na shida ya kuwapata watumishi au watenda kazi wazuri, maana kila mtu atajuwa wito wake na bila kusukumwa wala kubembelezwa, atawajibika mwenyewe, hoo haleluya!
Nikiwa nachukuwa digrii yangu ya Biblia, moja ya somo lililonigusa sana ni la kusifu na kuabudu. Niliguswa sana na kufuatilia kwa ukaribu habari za mmoja wa wandishi wazuri wa vitabu vizuri vya kiroho dunia na aliyetunukiwa tuzo mbalimbali za heshima, Dr. Aiden Wilson Tozer (April 21, 1897 - May 12, 1963). Katika kitabu chake kiitwacho Ibada: Hazina iliyosahauliwa katika kanisa, alisema: “ Kusudi la Mungu kumleta mwanae afe na kufufuka aketi mkono wake wa kuume, ni ili aturejeshee ile hazina iliyopotea, ile hazina ya ibada: Ili turudi na kujifunza kufanya tena kile ambacho tuliumbwa kukifanya tangu mwanzo: Kumwabudu Bwana katika uzuri wa utakatifu….Tuko hapa ili kwanza tuwe watu wanaoabudu na kuwa watendakazi ni jambo la pili”
Narudia tena kusema, ibaba ndiyo wito wetu wa kwanza kwa kila mwamini katika kila taifa “Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu (Kuabudu) mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa” (Ufunuo 15:4)
Daudi anasema “Na wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli “(Zab 22: 3). Katika tafsiri nzuri ya Amplified Bible inasema “But You are holy, O You Who dwell in [the holy place where] the praises of Israel [are offered]. Sasa niruhusu nikufafanulie kidogo hapa! Kuketi huko kwa Mungu kunakozungumziwa katika mstari huo, kwa kiebrania kunamaanisha Yashab (Yeu – Shab), yaani ni kuketi, kuishi mahali fulani, kudumu mahali fulani, kukaa, kuendelea, kuishi, kutembelea mara kwa mara, kufanya makao, kujificha au kujibanza mahali, kubaki mahali, kurejea au kungojea.
Ina maanisha, ukitaka kumuona Mungu na ukuu wake, wema wake, mafanikio yake, neema yake, rehema zake, fadhili zake, ebu jawa na sifa zake ; maana Yeye hukaa (inhabit), hudumu/huishi juu ya sifa za watu wake, na maali alipo Mungu hapo pana kila jawabu. Shida ya wakristo wwa kizazi hiki, wanakimbilia majawabu, ishara na miujiza bila kuzifuata kanuni za ki-Mungu; matokeo yake watu wamenyweshawa au kulishwa vitu vya ajabu. Acha kutangatanga, sio kila nabii, mtume au mchungaji ametokana na Mungu. Naamini, ukijawa sifa za ki-Mungu, ukawa mwaduo halisi, hakika huwezi kujichanganya.
Katika matendo 13 :1-2 “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho mtakatifu akasema, nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia “. Hapo kulikuwa na manabii na waalimu katika kanisa. Hapa tunaona kwamba kipaumbele cha huduma hakikuwa kutoa unabii au kufundisha, bali “ ibada “. Ni kwamba kila mtu alikuwa akiabudu, ndipo kutoka kwenye huduma ya ibada likatoka neno la unabii.
Hii inamaanisha tunapojawa na mioyo ya sifa na kuabudu, Mungu mwenyewe katika utatu mtakatifu hujihudhurisha pamoja nasi, huongea nasi, hutuhimarisha na kututenga kwa ajili ya huduma (utumishi au kutumika), maana Mungu wetu ni wakuabudiwa na kutumikiwa. Haisaidii kuwa na huduma kubwa wakati wewe mwenyewe huna moyo wa ibada, huduma hiyo itakuwa ya kukunufaisha wewe na sio Mungu wetu, Ndio maana katika kizazi hiki watu wameweka masharti mengi ndipo wamsifu Mungu; Mungu hayupo katika hilo na wala huwezi kusema umefanikiwa kwa hizo baraka za kuweka masharti ndipo upande madhabauni, lakini pia Kumbuka Mungu wetu ni Mungu mwenye wivu.
Katika kitabu cha Zekaria 14 : 17 anasema “ Tena itakuwa ya kwamba mtu awayeyote… asiyekwea kwenda Yerusalemu ili kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi, mvua haitakunya kwao “. Hapana ibada-Hapana mvua”, inaamaana tusipokuwa na mioyo ya kumsifu na kumwabudu Mungu, mvua ya baraka haiwezi kamwe kunyesha juu yetu, maana Yeye hukaa juu ya sifa.
Ukisoma (Ezra 1:1-11), Taifa la Israeli baada ya kuishi utumwani huko babeli, baada ya utawala wa mfalme Nebukadreza kuwatesa na kuharibu kabisa nchi yao, kuvunja ukuta, kubomoa makazi yao pamoja na hekalu na kuchukuwa baadi ya watu mateka pamoja baadhi ya vitu muhimu katika nyumba ya Bwana, lakini muda ulipowadia, Bwana akamwamsha roho mfalme Koreshi aliyetawala wakati huo. Kwa ufupi nikwamba, mfalme huyo aliwaruhusu wana wa Israeli warejee kuijenga upya nchi yao, yaani Yerusalemu. Katika kujenga upya, mambo manne yalihitajika yafanyike
a. Kujenga ukuta (Ili kuwakinga na maadui)
b. Kujenga nyumba zao (kwa ajili ya kujihifadhi)
c. Kujenga hekalu (mahali pa kukusanyikia)
d. Madhabau (Kumwabudia Mungu)
Katika yote hayo, Mungu aliwataka waanze na jambo moja muhimu. Kwa mtazamo wetu wa kibinadamu hasa katika mfumo wa ujenzi, labda ingefaa sana kuanza na ukuta au nyumba ya kuishi. Lakini ukisoma Ezra 3:1-4, Mungu anaelekeza kwamba waanze kujenga madhabau
Mungu anataka sana kuwa na ushirika na Yeye kuliko kitu kingine, yaani kuwa na ibada na Yeye na hayo mengine atayazidisha (Luka 12:31). Madhabau ndipo maali pa uhusiano wa mtu na Mungu, ndio maali pa kutengeneza, maali pa kutua kila mzigo. Mwanadamu wa asili mara zote huwa na madhabau fulani katika moyo wake, hivyo tuspojenga madhabau ya Mungu basi tutajenga madhabau ya ibilisi.
Katika kitabu cha Danieli sura ya 3, Hapo tunawaona watu waliojua uwezo wa kumtumikia na kumwabudu Mungu (Dan 3:11-28). Kina Shadraka, Meshaki na abednego wanashutumiwa kwa kutokukubali kutumika na kuiabudu sanamu. Katika tafsiri moja ya King James inasema “They serve not your gods nor worship the golden image).
Mfalme Nebukandreza akaghadhibika kwa hasira kwasababu watu hao hawakutaka kuitumikia na kuisujudia sanamu (Dan 3:14-16). Nakumbuka jibu la wanaume waliomjua Mungu wao wanasema (Dan 3:7) “ Mungu wetu tunaye mtumikia atatuokoa na hilo tanuru liwakao Moto”. Lakini katika ule mstari wa 28, Mfalme anagundua siri ya kumtumiki na kubwabudu Mungu wa Mbinguni. Ninapomalizia kipengele hiki cha utangulizi, nataka uelewe jambo hili kwamba; kumsifu Mungu ni jambo lingine na kumwabudu ni jambo lingine tena muhimu sana, lakini pia kumtumikia ni jambo lingine. Mambo yote hayo matatu ni muhimu sana, hawa ni mapacha watatu.

Ni utangulizi tu, mengine kama:

1. Nini maana ya kusifu kuabudu na kutumika
2. Baraka na vikwazo vya kusifu, kuabudu na kutumika
3. Mambo muhimu ya kuzingatia katika maisha ya kusifu na kuabudu
4. Sadaka au dhabiu ya sifa
5. Maana halisi ya ibada au kuabudu
6. Umuhimu wa kuabudu
7. Chimbuko la ibada
8. Misingi ya kuabudu
9. Picha halisi ya ibada
10. Muziki katika kusifu na kuabudu
11. Kuongoza ibada au kipindi cha kuabudu
12. Mambo muhimu ya kuzingatia ili kuwa kundi bora la sifa na kadhalika utayapata ndani ya kitabu.

Nakupenda lakini Mungu anakupenda zaidi.


0 comments:

HEART OF WORSHIP

HEART OF WORSHIP