1 September 2012

MAKALA MAALUMU KUTOKA GAZETI LA TANZANIA DAIMA NA Happiness Mnale



DAVID ROBERT: Mkali wa Injili anayetesa Channel O na MTV base


KATIKA miaka ya nyuma muziki wa Injili ulidharaulika sana na mtu alipoonekana akiimba muziki huo alionekana kama kituko kwa sababu hakuna aliyekuwa anaguswa na nyimbo hizo.
Si kwamba kipindi hicho hapakuwa na waimbaji wazuri wa muziki huo, la hasha walikuwepo tena waliokuwa wanafanya vizuri pengine kuliko waimbaji wa leo wanaoimba nyimbo za Injili.
Katika miaka hiyo kulikuwa na waimbaji kama Ephraim Mwansasu, Faustine Munishi, Mungu Four, Ency Mwalukasa, Jeniffer Mgendi na baadaye akajitokeza mwimbaji kama Cosmas Chidumule aliyekuwa anapiga muziki wa dunia kabla hajageuzia kibao kwenye nyimbo za injili.
Miaka hiyo ilikuwa ni mara moja sana kusikia muziki wa injili ukipigwa katika kumbi za starehe kama baa, kwenye harusi na mahali pengine kwenye starehe.
Lakini leo hii upepo umebadilika ndivyo alivyoanza kusema mwanamuziki mahiri wa muziki wa injili nchini, David Robert, aliyeibuka katika anga la muziki huo mwaka 2002 na albamu ya Baba.
Katika albamu hiyo Robert ambaye ana sauti nzito alishirikiana vema na Godwin Gondwe mtangazaji wa ITV ambaye naye ana sauti ya zege au sauti nzito lakini yenye mvuto sana na kuifanya albamu hiyo kuwa na mvuto wa kipekee na kuweka imara katika anga la muziki huo.
Albamu hiyo iliyokuwa na nyimbo kumi iliwashika wengi na kila mpenzi wa nyimbo za injili kupenda kusikiliza nyimbo zilizokuwemo. Baadhi ya nyimbo zilizokuwamo katika albamu hiyo ni Baba, Niongoze, Ngulujangu iliyoimbwa kwa kinyakyusa na nyinginezo.
Kufanya vizuri sokoni kwa albamu hiyo kulikuwa kama kumemtoa kimasomaso Robert kwani mwaka 2003 aliingia studio na kufyatua albamu ya pili inayojulikana kwa jina la Kiganjani pa Mungu.
Albamu hiyo ambayo nayo ilibahatika nayo kufanya vyema katika tasnia ya injili na hivyo ikamlazimu Robert kurekodi video ambayo nayo ilibamba.
Albamu yake ya tatu ni Adui yangu ilikuwa na nyimbo nane, hakuna asiyejua kila kitu kinachotengezwa kwa ubora, hutumia gharama kubwa kukikamilisha.
Hata hivyo Robert alikaa na kutafari, kwa makini jinsi gani anaweza kurekodi video ambayo inaweza kuwa tofauti na video zilizotangulia. Jibu lake lilionekana kuwa ni kujiweka sawa katika fungu la fedha.
Robert aliamua kuzichambua nyimbo zilizo katika albamu hizo mbili na kufanikiwa kurekodi albamu moja aliyoipa jina la 'The Best Of David Robert'.
Mwanamuziki huyo anaeleza kuwa albamu hiyo ilirekodiwa katika mandhari ya kuvutia na mtaalamu wa masuala ya filamu kutoka nchini Ujerumani Daniel Uphaus kwa kushirikiana na Sye ambaye ni mtaalamu wa kuongoza filamu.
Wataalamu hao waliirekodi kwa makini albamu hiyo hali iliyopelekea kukubalika katika soko la kimataifa, ambapo tayari vituo vya Chanel O na Mtv Base waliiomba kwa ajili ya kuirusha katika runinga zao.
Ubora wa albamu hiyo ya The Best of David Robert umetokana na maandalizi ya miaka mitatu aliyoyafanya kabla ya kuchukua uamuzi wa kuingia studio na kutoa kitu hicho ambacho kinamvuto mkubwa.
Kukamilika kwa albamu hiyo kulichukua miezi minne na baada ya kurekodiwa aliipeleka kwa wataalamu wengine kabla ya kuingia sokoni. Katika kuhakikisha albamu hiyo inakuwa tofauti na albamu nyingine hasa za muziki wa injili nchini, Robert alisafiri mikoa mbalimbali kwa ajili ya kupata picha nzuri kutokana na ujumbe wa nyimbo husika.
Mikoa aliyofanikiwa kwenda kurekodi albamu hiyo ni Morogoro, Iringa, Arusha, Moshi, Pwani na Dar es Salaam.
Robert aliyezaliwa Machi 18, mwaka 1978 Mabatini, jijini Mbeya anasema kuwa huduma ya uimbaji alianza tangu akiwa mtoto, alipokuwa shuleni, ambapo aliifanya kwa nguvu zote kwa kutembelea shule mbalimbali kwa lengo la kutoa injili kwa njia ya nyimbo hiyo ikiwa mwaka 1998 wakati akisoma Shule ya Sekondari ya Jitegemee, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kuipenda huduma hiyo wapo waimbaji waliomvutia akiwamo Mchungaji Ephraim Mwansasu, Mchungaji Daniel Richard Mwansumbi na Cosmas Chidumule hao ndio waliompa hamasa kubwa Robert kujikita katika anga la muziki huo wa injili.
Waimbaji hao ndio walikuwa wakimvutia kutokana na sauti zao kuwa nzuri pamoja na ujumbe wa nyimbo uliokuwamo ndani ya nyimbo zao na mitindo waliyokuwa wakiitumia.
Kwa upande wa mafanikio kupitia muziki huo wa Injili Robert anaseama: “Nimefanikiwa kujenga nyumba nzuri ya kisasa, kumiliki gari lakini mafanikio mengine ni pamoja na kupata mtandao mzuri wa marafiki ndani na nje ya nchi na kuwa na miradi mbalimbali inayonisaidia kuendesha maisha yangu ya kila siku,” anasema.
Kwa upande wa changamoto, mwanamuziki huyo anasema kuwa anakabiliwa na mtaji mdogo wa kuitangaza huduma ya Mungu ndani na nje ya nchi, kutumia gharama kubwa katika kurekodi albamu na mwisho wa siku anajikuta mfukoni hana kitu, wapiga picha kuchelewesha kazi, ambapo kama alikuambia anakupa baada ya wiki mbili basi atakupa baada ya miezi miwili, masta hazina ubora na teknolojia kuwa chini, isiyokidhi ubora wa kimataifa na matatizo ya umeme usio wa kudumu pia huchangia kazi kusuasua.
Anasema kuwa anakerwa sana na waimbaji wanaokimbilia katika muziki huo kwa kuangalia masilahi ya pesa zaidi kuliko huduma.
Ambapo watu wengi wamekuwa wakijikuta wanashindwa kufanya vema kazi ya Mungu pindi wanachokitarajia kinanapokosekana.
Mwimbaji huyo mwenye mke na mtoto mmoja anasema wazi bila kificho kuwa muimbaji mwenzake anayetamba na albamu yake mpya ya ‘Nipe macho’, Christina Shusho, ndiye anayemvutia zaidi kutokana na nyimbo zake kuwa na ujumbe mzito ambao mara nyingi nyimbo hizo hugusa maisha anayopitia.
Kwa upande wa matarajio anasema kuwa anatamani kufanya mapinduzi makubwa katika muziki wa injili kwa siku za usoni. Mbali na hilo anatamani kuona muziki wa injili ukisambaa kimataifa zaidi na waimbaji wazalishe kazi zenye ubora wa hali ya juu.

0 comments:

HEART OF WORSHIP

HEART OF WORSHIP