7 May 2012

ASKOFU DKT. MOSES KULOLA AKEMEA UZAZI WA MPANGO, ASEMA HUKO NI KUMKOSOA MUNGU--



Wakati Serikali ikiendeleza mikakati ya kutoa elimu juu ya uzazi wa Mpango Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Dakta . Moses Kulola amepingana na sera hiyo na kusema ni kuingilia maamuzi ya Mungu. Kiongozi huyo alisema kuwa hakuna sababu yoyote ya serikali kuweka mikakati ya kutoa elimu ya kufunga kizazi kwani hiyo ni kazi ya Mungu mwenyewe.

Alisema kuwa kuna kila sababu ya kuikemea mipango hiyo kwani suala la kudai kuwa pawepo na uzazi wa mpango ni kuwa na hofu ambayo inasababishwa na shetani jambo ambalo ni hatari kwa taifa. “Mimi nilifyatua watoto kumi na sikushindwa kuwasomesha japo wapo watu ambao walikuwa wakisema kuwa watanishinda kuwasomesha.
 “Ninavyosema kijana mmoja wapo huyo hapo ni mtoto wangu huyo hapo mwenye kipara na huyo ni mtoto wa tatu. Ilipofikia wakati wa Mungu alizuia mwenyewe kwani aliona mke wangu amechoka. Acha kabisa masuala ya kushabikia mambo ya uzazi wa mpango kwani huo ni mpango kamili wa Shetani”, alisisitiza Dakta Kulola.

Aidha kiongozi huyo Mkuu wa Kanisa la EAGT aliwakemea watumishi wa serikali ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia wananchi. Hayo aliyaeleza alipokuwa akiongea na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) katika ibada ya shukrani iliyofanyika katika Kanisa la EAGT Siloam Ipagala Mjini hapa.

Askofu Dakta. Kulola alisema kuwa anasikitishwa na baadhi ya watumishi ambao wamekuwa wakijivunia vyeti vyao ambavyo vinaonyesha elimu walizo nazo lakini wanashindwa kutimiza wajibu wao pindi wawapo ofisini. Kiongozi huyo alisema kuwa wapo baadhi ya wasomi ambao wanachukua masomo yao kutoka nchi za nje, lakini cha kushangaza pindi wanaporudi nchini wanashindwa kufanya kazi zao kama inavyostahili .

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi amewataka wasomi wa Vyuo Vikuu nchini kuwa mfano katika jamii tofauti na ilivyo sasa. Alisema kuwa wasomi wengi ambao taifa linawategemea wamegeuka kuwa vituko kwani wasomi wengi wa Vyuo Vikuu wamekuwa wakiongoza kuingia katika klabu za mziki na kufanya mambo ya anasa.
“Inasikitisha kuona wasomi ambao taifa linawategemea kujihusisha na vitendo vya ajabu, kutokana na vitendo hivyo inatia hofu pindi wakiingia kazini. “Nataka kuwaambia wanavyuo kamwe hamuwezi kuheshimika katika jamii kama mtaendelea kulewa, kujiingiza katika anasa kama inavyofanyika kwa sasa” alisema Dk.Nchimbi.

0 comments:

HEART OF WORSHIP

HEART OF WORSHIP